Wanasayansi mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki wamekuwa wakitafiti juu ya uwezekano wa kutumia teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) katika kilimo.
Hatua hii inatokana na teknolojia hiyo kuwa na upinzani kwa kile kinachoelezwa kuwa ikitumika inaweza kusababisha athari za kiafya na mazingira. Hata hivyo, watafiti mbalimbali duniani wamekuwa wakiitetea teknolojia hiyo kuwa ni salama na tayari baadhi ya nchi kama vile Marekani, India na China zimeshaanza kutumia teknolojia hiyo katika kilimo.
Uzuri wa GMO
Uzuri wa teknolojia ya GMO ni kwamba inaweza kumsaidia mkulima kuvuna mazao mengi katika eneo dogo, kutotumia au kutumia kidogo dawa za kuulia wadudu na mazao kumea vyema kwenye maeneo yenye mvua kidogo. Nchi mbalimbali zimekuwa zikitamani kuona wananchi wake wanazalisha chakula cha kutosha na pengine kuwa na ziada kwa ajili ya kuuza, lakini zimekuwa na hofu ya kujiingiza kichwa kichwa kwa kuwa ni teknolojia mpya.
Mfano mzuri ni Rais Jakaya Kikwete alipotembelea Taasisi ya Tafiti za Kilimo ya Mikocheni (MARI), Machi mwaka huu na kuhimiza wanasayansi kuharakisha utafiti wa teknolojia ya GMO, ili Watanzania waanze kuifaidi. Alisisitiza kwa kusema: “ Umefika wakati kwa Watanzania kubadili mawazo hasi juu ya teknolojia hiyo, kwa sababu tafiti mbalimbali duniani zinaonyesha ni salama hasa ikizingatiwa kuwa hadi sasa hakuna uthibitisho wa kisayansi unaoonyesha kuwa GMO ina madhara kwa afya ya binadamu.”Kimsingi, Rais Kikwete alisema Serikali ipo tayari kuweka sera ya matumizi ya teknolojia hiyo mpya kwa nchi nyingi duniani, lakini itafanya hivyo baada ya watafiti wake kutoa ripoti kamili kuhusu teknolojia hiyo na kushauri kulingana na uchunguzi wao.
Tafiti za GMO Tanzania
Wanachofanya wanasayansi kupitia teknolojia hii ya uhandisi jeni ni kutumia mbinu za kibiolojia za maabara, ili kupunguza au kuongeza tabia ama faida ya mazao ya mmea au mnyama. Marekebisho hayo hutegemea mahitaji yaliyolengwa na mtafiti.Miongoni mwa mabadiliko ambayo mtafiti anaweza kuyatekeleza kupitia teknolojia ya GMO ni kufanya mazao kuwa na lishe bora zaidi, uwezo wa mmea kukabili magonjwa, wadudu waharibifu na mmea kuweza kukua katika mazingira ya mvua kidogo.
Mtafiti Mkuu wa Kituo cha Utafiti na Udhibiti Magonjwa ya Mimea ya Kitropiki (TPRI), Dk Roshan Abdallah anasema Tanzania haijaanza kutumia GMO wala kuruhusu mazao yaliyozalishwa kwa teknolojia hiyo kuingia nchini. Ili kujiridhisha juu ya faida na hasara ya teknolojia hiyo, anasema Serikali kwa kutumia kituo hicho, inafanya uchunguzi kuhusu usalama wa Watanzania iwapo GMO itatumika. Kwa sasa uchunguzi huo upo katika ngazi ya maabara.
Hatua hiyo anasema itafuatiwa na majaribio ya mimea iliyozalishwa kwa GMO na kulimwa kwenye mashamba maalumu yenye udhibiti katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, anasema nchi zote zinazopakana na Tanzania zipo mbele zaidi katika utafiti wa GMO na huenda zikaidhinisha itumike, hivyo kuipa Tanzania wakati mgumu katika kudhibiti mazao ya namna hiyo kulimwa au kutumika nchini.
Tafiti za GMO Uganda
Wakati Tanzania ikiwa kwenye hatua hiyo ya awali, nchi jirani ya Uganda tayari imeanza majaribio kwenye maeneo mbalimbali. Miongoni mwa mazao hayo ni mihogo, pamba na ndizi.
Mkuu wa Kituo cha Bioteknolojia ya Kilimo cha Kiwanda kilichopo nje kidogo ya jiji la Kampala, Dk Andrew Kiggundu, anasema wameanza utafiti wa majaribio ya GMO kwenye mashamba tangu mwaka 2010 na wanatarajia kukamilisha utafiti huo mwaka 2020.
“Tunatarajia ifikapo mwaka 2020, tutakuwa na majibu mazuri, pengine wakulima kuanza kuruhusiwa kuitumia ili kuongeza uzalishaji,” anaeleza.
Kwa sasa anasema wanajaribu kuchunguza mwenendo wa ukuaji pamoja na kujiridhisha juu ya uwezo wa mazao hayo kuweza kukabiliana na magonjwa ya mimea pamoja na wadudu waharibifu. Baada ya hatua hiyo, anasema watafanyia majaribio mazao hayo kupitia panya na kuchunguza mwenendo wa afya zao. Watatumia panya kwa sababu kisayansi mfumo wao wa kiutendaji unafanana na wa binadamu, kwani athari zozote zinazoweza kujitokeza kwa wanyama hao pia zinaweza kumpata mwanadamu.
Dk Kiggundu anasema wakijiridhisha kuwa mazao hayo hayana madhara kwa panya, utafiti wao utawakuwa na majibu kwamba ni salama kwa afya ya Waganda. Akizungumzia teknolojia hiyo kupitia shamba la migomba iliyokuzwa kwa GMO, Mtafiti Mkuu wa kituo hicho, Dk David Talengera, anasema wametumia teknolojia hiyo katika aina ya migomba inayopendwa na watu wengi, ili kuzalisha mazao ambayo yatakuwa na faida zaidi kwa Waganda.
Dk Talengera anasena kwa ujumla utafiti huo unaendelea vizuri na wana imani watafikia hatua ya majaribio kwa wanyama miezi ya karibuni. Hata hivyo, anasema kwa sasa mazao yote wanayozalisha kwenye shamba hilo yamekuwa yakiteketezwa katika mpangilio maalumu ambao wanahakikisha hayatumiwi na binadamu, wanyama na wadudu. Ili kuzuia ndege au nyuki kuchukua chochote kwa ajili ya chakula ama kutengeneza asali, anasema wamekuwa wakifunika mikungu kwa mifuko. Mkemia katika Maabara ya Taifa ya Utafiti wa Kilimo Nchini Uganda, Nuwamanya Ephraim anasema wanasayansi wa Afrika Mashariki wana kawaida ya kubadilishana uzoefu, hivyo anaamini watakayobaini kupitia tafiti hizo ni faida kwa eneo zima la Afrika Mashariki.
Katika Afrika nchi ambazo tayari zimeruhusu teknolojia ya GMO itumike katika kilimo ni Afrika Kusini, Burkina Faso, Misri na Sudan. Nje ya Afrika nchi zinazotumia teknolojia hiyo ni pamoja na Marekani, Argentina, Brazil, Canada, China, Paraguay, India, China, Mexico, Romania, Ujerumani na Ureno.
credits: mwananchi
No comments:
Post a Comment